NI ZAIDI YA KITCHEN PARTY
By Zubagy Akilimia
Kwanza kabisa napenda kuwapa HONGERA wanawake,
sina budi kufanya hivyo ikiwa ni ukweli usipingika mwanamke ni kocha mchezaji
wa familia mwenye umuhimu hasa kufundisha watoto, mumewe na hata majirani
inapobidi. Kimsingi familia bila mwanamke bado haijasimama, lazima kiongozi wa
pili awe mwanamke, kwani siku zote
tunafahamu kiongozi mkubwa ni baba!
Pamoja na baba kuongoza familia, naye
huongozwa na mwanamke na akabadilika iwapo tabia yake inakuwa ndivyo sivyo.
Mfano mzuri, wapo wanaume ambao kabla ya kuoa
walikuwa na tabia chafu hasa ya uzinzi, uasherati, wizi, uvuvi wa kufanya kazi,
ufujaji wa pesa, walevi na hata wavutaji sigara lakini siku chache baada ya
kuoa, walibadilika na kuacha mambo mabaya waliyokuwa wakiyafanya. Sababu ni nini?
Mwanamke alifanya kazi hiyo. Hapo utakubaliana nami, kuwa mwanamke bado ni
kiungo muhimu na kiongozi wa familia.
Zaidi mwanamke ana sifa kubwa sana ambayo
huwezi kuifananisha na kitu chochote ndiyo maana wengi wanasema ‘mama ni mama’,
nafahamu kiasi gani mwanamke anavyopata suluba nyingi maishani mwake, ndiyo
maana wengi wanasema mama ni kila kitu. “Mama is the best’. Kuanzia leo
mwanamke jisikie wewe ni zaidi ya kila kitu na majukumu uliyonayo ukiyafanya
ndivyo sivyo na kwenda arijojo utakuwa
umeharibu familia nzima.
Mwanamke amekuwa akiteseka wodini wakati wa
kujifungua, usiku kulea mtoto. Siku zote anapoteza nguvu zake kumnyonyesha
mtoto, kumuogesha, kumvisha, kumlisha na mambo mengine kibao, huku pia akiwa
mwalimu wa familia hasa kwa watoto.
Ni
jambo la kusikitisha sana. Zaidi mwanamke wengi hufia wodini wakati wa
kujifungua kwasababu ya presha na kutokwa na damu nyingi hasa wale
waliokeketwa.
Kutokana na hilo nasisitiza mwanamke ni
bora na kiungo kiongozi wa familia.Baada ya hayo machache, mpenzi msomaji nachukua
sekunde hizi kuzungumzia somo letu la ZAIDI YA KITCHEN PARTY. Katika kitabu hiki
ni imani yangu wewe mwanamke utabadilika na kuwa mke bora ndani ya ndoa yako.
KUMTUNZA MUMEO
Huenda wengi wanaweza kushtuka pale wanapoona
neno ‘kumtunza mumeo’, wanawake msishtuke kwani wengi siku zote mmezoea kusikia
mwanaume ndiye mwenye jukumu la kutunza mwanamke, lahashaa! Tunakosea sana
wengi wetu! Fahamu kuwa nawe pia una kila sababu ya kumtunza mwandani wako.
Mbali na kulea familia, hasa watoto! Mwanamke
unapaswa kumlea ‘mtoto mkubwa’ ambaye siku zote unambeba nyakati za usiku! Huyu
unapaswa kuhakikisha anakuwa safi na mwanaume bora mbele ya jamii.
Najua wapo wanawake wengi wanashindwa
kuwajali wanaume zao na kuwaacha kama kuku wa kienyeji, bibie utachekwa!
Hakikisha mumeo anakuwa ‘smart’ maridadi
mwenye mvuto hata kwa macho, acha akuvutie uzidi kumpenda.
Usijaribu kumuacha ‘rafu’, wanawake wengi
wanapoolewa wanawaachia house girl wawatunze waume zao, kuanzia kuwafulia nguo
zao, tena bila woga huwaachia hadi zile nguo za ndani.
Loh! Mwanamke unapofanya hivyo unabomoa
ndoa yako kwa mikono miwili, utakapoona mumeo anaanza tabia ya kujichekesha na ‘house
girl’ wako unadhani nini kinaendelea? Unaanika aibu yako! Nguo za ndani
hakikisha unafua mwenyewe! Tena si vema kuziweka hadharani, mnajidhalilisha
wenyewe! Hakikisheni mnazificha kama mnavyoficha sehemu zenu za siri.
MWANDAE MWANAUME!
Nikisema mwanamke unapaswa kuamuandaa mumeo, simaanishi
kimapenzi, mbali na kulea familia unajukumu la kuhakikisha unamlea vema ‘husband’
wako na kumtunza kwa kila kitu licha ya kwamba nawe unategemea matunzo muhimu
na bora kutoka kwake.
Ninaposema una kazi ya kumwandaa, nazungumzia swala la mavazi,
kabla mumeo hajatoka chumbani hakikisha ameshavaa nguo safi zinazoendana na
viatu, suruali na shati. Tumia muda mwingi kumchagulia nguo gani anapaswa kuvaa
ofisini, wakati wa mtoko ‘OUT’ siku za ‘wikiendi’ nk.
Zaidi ya hayo, nirudi katika ulimwengu wa mapenzi,
mwanamke pia ana jukumu kubwa la kuhakikisha ndoa yake inadumu na anaiboresha
zaidi kuliko kitu kingine. Je, anaiboreshaje ndoa yake, na ni mambo gani ya
kufanya chumbani? Peruzi nikujuze...
USISUBIRI MWANAUME AKUOMBE!
Katika karne hii ya 21, ndoa zetu za wajanja wa mjini zimekosa
nguzo imara, mara nyingi watu wamejiandaa kwa ‘harusi’ sherehe za ndoa lakini sio
ndoa halisi, wanafanya fasheni kuoana bila kujua ndoa inahitaji kuimarishwa.
Huwezi kupanda mmea jangwani ukategemea utaota pasipo maji, mbolea nzuri na
hewa?. Jibu ni NO! Hali kadhalika, ndoa nayo inahitaji vitu vingi sana.
Wanapoingia na
kuwa wake halali wanasahau wajibu wao wa kutii sheria za ndoa za jamii yetu
husika kwa ujumla.
Wanawake wengi wa ndoa ambao mara nyingi
hawataki kujifunza wamekuwa kero sana kwa waume zao.
Unajua kwanini? Kwanza tangu kuolewa kwake
hajawahi kumuomba mumewe mapenzi, licha ya kusumbuliwa na hisia za kuhitaji
kitendo hicho anajikuta akiona aibu, woga na kujikuta akisubiri hadi mwanaume
amwambie. Jamani, kufanya hivyo siyo poa! Haya, hivi mumeo naye akachuna ni
kwamba utakaa tu kama boga la shambani? Hebu tukae na kufikiria suala zima la
kuridhishana.
Wakati mwingine ‘ubize’ wa kazi unaweza
kumsahaulisha mwanaume majukumu ya kiunyumba, ni wewe mwanamke unayepaswa
kuomba penzi. Tena unapoomba hakikisha unashawishi wako katika mavazi umepitiliza,
vaa nguo fupi zilizokuacha wazi, muonyeshe maeneo yako muhimu unayojua kabisa
yanaweza kumdatisha na kujikuta akiungana naye kuutipisha usiku murua.
Usisubiri tu, kwani huna haki ya kuomba
penzi, tena niwafundishe kitu. Ili kumkamata vema mume wako lazima uwe mjanja,
hakikisha unamuonyesha mapenzi yote! Mfanye akutamani kila mara.
Zipo njia nyingi zinazoweza kumfanya
mwanaume akuone bora, kuwa karibu naye na mfanye rafiki yako na hata kuomba
ushauri kila unapoona jambo fulani linakutatiza.
Kumnunulia zawadi ndogo ndogo ambazo kila
anapokuona anajidhihirishia penzi lako la ukweli na si la kitapeli, jifunze
kuwa na kauli nzuri, mambo ya kuropoka ama kumfokea mumeo utadhani mwanao acha!
Acha kabisa, jaribu kulainisha mdomo wako utoe maneno matamu yenye harufu ya
mahaba, angalia sio poa unajaribu kumpanda mumeo kichwani, kufanya hivyo ni
ulimbukeni.
Nishangaa sana kusikia mwanamke
anamlazimisha mumewe afanye mambo yasiyo na msingi.
Yupo dada mmoja aliolewa maeneo ya Sinza
Kwa Remmy, tabia yake haikuwa nzuri sana,wivu wake ulipitiliza, kila mumewe
alipotoka kazini, hakuruhusiwa kuingia chumbani na nguo, kwa amri aliamrishwa
kuvua nguo punde anapoingia chumbani na kuziacha hapo chini, na mkewe kuanza
kuzinusa na kuzikagua.
Hakuwa akimwamini mumewe, sasa ni mateso
gani hayo? Hiyo siyo fresh! Mpe uhuru wa maisha yake na si kumkaba kiasi hicho,
unadhani ukifanya hivyo ndiyo kumzuia asitoke nje? Fikiria na unapogundua mumeo
ana tabia ya kukusaliti, hakikisha unarejesha penzi kwa kuongeza mapenzi na
kumfanya awe karibu yako kuliko kitu chochote.
EPUKA NENO ‘SIJISIKII’
Ni maajabu sana mwanamke kumwambia mumewe ‘sijisikii’. Kwanza kauli hii si nzuri na iwapo unahisi
huhitaji kujumuika na mwenza wako, tumia lugha laini unayohakikisha itamridhisha
na kumfanya asitoke nje.
Iwapo unamwambia hujisikii bila kunyumbulisha kutojisikia kwako ni rahisi
kuanza kukufiria huenda kuna mahala unapata huduma hiyo ndiyo maana unamtosa
kila siku kwa kusema ‘sijisikii’
Wanaume wengi wamekuwa wakinieleza maudhi na kero ambazo zimekuwa haziishia
ndani ya ndoa, wengi wanadai wanapowataka wanawake zao kimapenzi hudai
‘Hawajisikii’ na ‘wamechoka’.
Kauli hizo zimekuwa zikiwafanya watafute mahala ambapo wanaweza kupata
furaha, ni kweli wanaume wengi wao hawapendi usumbufu hasa wanapohitaji furaha
na mapenzi.
Hata unapokuwa kwenye hedhi, yapo mambo unayoweza kumfanyia ‘sweetie’ wako akafurahi,
akina dada wengi wanajua mapenzi lazima wakutane kimwili, siyo kweli. Fahamu kitendo
cha kufanya ‘romance’ pia huchangia na huboresha penzi, licha ya kwamba wapo
wanapofanya ‘romance’ hutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi. Ipo michezo ya
kujumuika pamoja.
Usimbanie mumeo, utajikuta ukiingia kwenye maumivu ya
kujitakia.
Maisha yana hatua nyingi hadi kufikia utu uzima, hatua
kubwa na nzuri kabisa ambayo wengi wanaipitia ni maisha ya ndoa. Ni kitu muhimu
na ndoto ya kila mtu,lakini kwa mwanamke ,akiwa kama mlezi, mlinzi na mwenye
wajibu mkubwa wa kuhakikisha maisha
yanakwenda salama anatakiwa kuwa makini na ndoa.
Lakini bahati mbaya, wengi wa wasichana wa siku hizi
wanachukulia kitendo cha kuolewa kama fasheni, ujiko au dhihirisho kwamba wao
no wazuri wa sura, umbo au wajihi na hivyo kwao kuolewa ni zawadi ya kufanya
wawakebehi na kuwadharau wenzao ambao
hawajapata bahati ya kuolewa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni