MAFIA WA BONGO (1)
Mwandishi, Zubagy
Akilimia, 0712313191
Ukimuona kwa jinsi alivyo unaweza
kusema si Mtanzania halisi, hii ilitokana na urefu wake wa futi saba kasoro na weusi uliopitiliza. Kwa
kumtazama ungeweza kusema ni Mkikuyu kutoka Kenya au rai wa nchi jirani ya Rwanda.
Pamoja na kwamba alikuwa na umri wa miaka 17, ungemkisia kwa kusema ana miaka
30. Umbo lake liliweza kutisha wanaume wengi wavimba mbavu mbili na kuwavutia
wasichana wenye kupenda mwanaume mwenye mwili mkubwa.
Kijana huyu jitu la miraba
mnne alizaliwa Tarime vijijini na kukulia huko huko Mkoani Musoma.
Wakati anazaliwa alikuwa
na kilo gramu nne na nusu(kg 4.5).Mtoto huyu kwanza alichelewa sana kutembea na
hata kuongea, wazazi wake awali walidhani wamepata mtoto bubu na mlemavu, haikuwa
hivyo kwani baadaye akiwa na miaka miwili aliweza kutembea na kuongea vizuri
Kikuria.
Utaalamu wake mkubwa, ni kupiga shabaha na ujuzi wa
kuzaliwa nao ulikuwa kukarabati bunduki aina ya ‘Gobole’ na Bastola aina zote
na hata ‘Machine Gun’.
Watu wengi wanafahamu wazi watu wanaoweza kutengeneza au
kukarabati bunduki mara nyingi ni waliopitia mafunzo wa kijeshi, kwa upande wa Masato
Lwegambura watakuwa wamekosea.
Kijana huyu si miongoni mwa watu waliopitia jeshi, ingawa
alitisha na kuonekana zaidi ya mtu aliyepitia mafunzo ya jeshi. Huu ni uwezo
binafsi uliowashangaza hata askari waliokuwa wakimtafuta kwa ajili ya kumtia
mikononi mwa polisi.
Wengi walihisi huenda anatumia dawa za kichawi, kutokana
na uwezo wake wa kuua na kutokomea bila kukamatwa.
Unaweza kujiuliza kichwani mwako.Je, huyu kijana mdogo
ameweza kupata wapi ujuzi wa kukarabati, kutengeneza silaha na kuzitumia, sasa
ukakuna kichwa na kuguna. Mhh!.
Ukweli, historia ya Masato ni nzito sana, ni kijana aliyelelewa
na babu yake mzee Simon Lwegambura, baada ya baba na mama yake kuvamiwa na
kuuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kuchoshwa na ujambazi wa baba yake.
Kifo hicho ndicho kilichosababisha Masato kuwa yatima na kutowafahamu wazazi
wake. Babu yake alimchukua mjukuu huyu na kwenda naye kijiji cha mbali na mjini,
awali familia ya Lwegambura ilikuwa ikiishi Musoma mjini maeneo ya Mwembeni.
Masato akiwa na umri wa miaka mitatu aliishi kiseja na babu yake ambaye hakuwa
na mke wala mtu mwingine wa kumsaidia. Aliishi na Masato akimpikia uji, maziwa
ya Ng’ombe maana alikuwa mfugaji mkubwa wa Ng’ombe.
Kutokana na ukorofi wa mzee Simon Lwegambura, hakuna
jirani aliyekuwa anamsogelea, mara nyingi marafiki zake walikuwa viongozi wa
nchi jirani na matajiri ambao walifika nyumbani kwake asubuhi sana au usiku
wakiwa na magari.
Hakuna aliyeelewa mzee Simon alikuwa akifanya biashara
gani na viongozi na matajiri hao. Kuna watu walianza kusema huenda mzee Simon
ni mpelelezi maana hata magari ya vigogo yalifika kwake na kuondoka. Tetesi
zikaenea mtaani, na kumfanya Mzee Simon aigopwe sana kijijini kwao. Wageni
mbalimbali ambao hawakujulikana walikotoka walifika na kuondoka kisha kurudi
tena na kilichowashangaza wengi ni ile hali ya mgeni kuwa lazima akienda arudi
tena.
Kilichomsaidia watu wengi kushindwa kumuelewa kazi halisi
ya Mzee Simon, ni kule kutopenda kuzoeana na hata wazee wenzake. Zaidi ya
salamu, hakuna mazungumzo mengine.
Ufinyu wa kutozoeana ukazidi kuwatia watu wasiwasi,
wengine walimuona huenda ana uwendawazimu kama si laana.
“Haiwezekani mnaishi na mtu hata hana mazoea wala haendi
kwa mtu, yeye rafiki zake ni wageni…” Mzee mmoja alilalamika, akajaribu
kujipendekeza akachoka maana mzee Simon hakutaka mazoea.
Rafiki yake mkubwa mzee Simon ni mjukuu wake, hata
alipoanza shule ya msingi, majirani na watu mbalimbali walianza kumchunguza
Masato na kutaka kujua ukweli wanavyoishi na babu yake.
“Masato, nyumbani nani anakupikia chakula?”
“Chakula, tunapika na babu…”
“Ahaa! Kwa hiyo hakuna mtu anayeishi na ninyi?”
“Hakuna tupo wawili tu…”
“Safi sana, na wale wageni wanaokuja na kuondoka wanaleta
nini au wanakuja kuchukua nini?” Huyu alikuwa ni mjumbe wa nyumba kumi aliamua
kumfuatilia Masato shuleni.
“Hakuna kitu, wale ni ndugu zetu…”
“Ahaa, mbona wanakuja na kuondoka hawalali?”
“Hakuna nafasi ya kulala, sisi tuna vitanda viwili tu…”
“Sawa, babu yako anafanya kazi gani ndani?”
“Hana kazi, anapenda kusuka ukili tu…” Masato
alidanganya, kumbe mzee huyu ambaye ni mjumbe hakujua kama Masato alishapewa
elimu na babu yake kuhusiana na watu watakaotaka kumpeleleza.
Akili yake ilishalifahamu hilo mapema ndiyo maana
alimfundisha maisha ya ukubwa na jinsi ya kujibu maswali na hata kujitetea.
Baada ya kupeleleza huo wa muda wa dakika kumi, hatimaye
Masato alienda shuleni na kuingia darasani. Hata hivyo, pamoja na kuwa darasani
akimsikiliza mwalimu kwa makini, somo la babu yake ndilo alilolipenda zaidi
kuliko la darasani.
Akiwa na umri wa miaka kumi na moja, darasa la tano
Masato alishafahamu kusafisha bunduki maarufu kwa jina la ‘Gobole’, Bastola za
kila aina, mfano Revolver, M92 Beretta, Short Machine Gun(SMG) nk. Alipofikisha
umri wa miaka 13, babu yake ambaye kazi yake kubwa ilikuwa kukarabati na kutegeneza
silaha kwa siri bila jeshi la polisi kufahamu, alimfundisha ufundi wa
kukarabati silaha zote.
Kutokana na kuipenda kazi hiyo na kupenda kutumia bastola,
Masato akawa mtaalam na hata zilipoletwa bastola za kusafisha na kutengeneza
aliweza kuifanya kazi hiyo kwa ubora wa hali ya juu. Babu yake alishangaa sana
na upendo kwa mjukuu wake ukaongezeka maradufu. Akili mwake, alifahamu amepata
mrithi wa kazi yake, jambo lililompa faraja.
“Umesikia mjukuu wangu, hii ni kazi ninayoifanya kwa
magendo, sipendi mtu yoyote ajue zaidi ya wateja wangu,” ilikuwa sauti ndogo
huku akimshika kichwa na kuchezea nywele zake.
“Nimekuelewa babu, na ukweli babu hii kazi naipenda sana.”
“Nashukuru kusikia hivyo. Ila nakuonya…usije kuiga kazi
ya baba yako…”
“Kazi gani?” Masato akamwangalia babu yake kwa udadisi.
Hakujua kama baba yake alikuwa jambazi sugu na Mafia wa Bongo.
“Baba yako alikuwa jambazi hatari sana Tanzania hii,
nilipenda awe mwanajeshi kwa ajili ya kutetea rai na aridhi yetu ya Tanzania,
kumbe alipokwenda jeshi alienda kwa nia ya kujifunza uwezo wa kuua, kutumia
silaha za kivita na ufundi mwingine wa shabaha…”
“Dah! Baba yangu alikuwa Mafia! Kama akina Van Damme,
Bruce Lee?”
“Zaidi, kwani Van Damme na Bruce Lee walikuwa wanaigiza
filamu tu…yeye alikuwa anafanya kweli, akisema naua leo lazima aue kweli,
akisema navamia duka na kupora pesa lazima afanye hivyo,” yale mazungumzo
yalimvutia sana Masato bila mzee Simon kuelewa kuwa alikuwa anamharibu mjukuu ubongo
wake. Alipenda sana kutumia bastola kuliko kiumbe yoyote duniani.
Kadri siku zilivyozidi kwenda, umri wa babu ulizidi
kumtupa, kazi nyingi zilikuwa zinafanywa na Masato. Kitu kikubwa ambacho
kiliwashangaza majambazi wengi, ni ile hali ya shabaha na uelewa wa kutengeneza
bunduki kwa kutumia miti na vyuma.
Kuna wakati majambazi wa Mwanza wa Kundi la Jembe
walifika Tarime kwa ajili ya kumuomba Masato aweze kujumuika nao. Kijana huyu
aligoma kabisa, maana alipewa historia ya kifo cha baba yake.
Hata hivyo, alipenda sana kutumia bastola na ataitumia
wapi, kama siyo kwenye matukio ya ujambazi? Hili lilikuwa ni zoezi gumu sana
kwake.
“Babu, naomba unifundishe ujuzi mwingine maana naona wewe
sasa hivi umezeheka sana…” Masato akiwa na miaka 17 alimweleza babu yake.
“Kitu ambacho nimekuwa sijakufundisha ni kutengeneza
baruti na mabomu ya kutupa kwa mkono, na itabidi ufahamu vitu vya kutengenezea
na adhari zake kabla ya kuanza zoezi. Itabidi twende msituni ili kunifundishe
zaidi,” Babu mtu alimwambia mjukuu wake, alishaelewa kuwa siku yoyote anaweza
kuaga dunia.
Huu ni mwanzo tu,
hadithi ndiyo kwanza inaanza. Fuatilia ujue Masato amefanya mambo gani? Usikose
kusoma kitabu changu cha WANAWAKE WAZURI MATESO, kinauzwa TSH 4000/= Kwa wauzaji wa magazeti nchi nzima.